HAKIKA UTAMU WA MECHI YA STARS NA BOTSWANA ULINOGESHWA NA MATUKIO HAYA HAPA.




Na. Melkiory Gowelle.
 
WAKATI ratiba ya FIFA kwa mechi za kirafiki za kimataifa ikiendelea, Jana march 25, 2017 katika uwanja wa Taifa, tulishuhudia kandanda safi lililopigwa kati ya wenyeji timu ya taifa ya Tanzania ‘Taifa stars’ dhidi ya timu ya Taifa ya Botswana ‘The Zebras’.

Kama kawaida katika mchezo wa soka huwa hakukosekani matukio mbalimbali, hivyo Basement255 imekukusanyia matukio yote yaliyo tokea kabla na baada ya mechi hiyo, ambayo yalikuwa chachu ya ushindi kwa ‘Stars’ lakini pia yaliongeza furaha kwa mashabiki na wapenzi waliokusanyika kushuhudia mtanange huo. 

MABADILIKO YA BENCHI LA UFUNDI.
Katika mechi hiyo Stars iliingia uwanjani ikiwa na mabadiliko makubwa katika benchi lake la ufundi, ambapo iliongozwa na kocha mkuu Salum Mayanga ambaye alirithi mikoba kutoka kwa Charles Boniface Mkwasa ‘Masta’, ambaye kwasasa ni katibu mkuu wa Dar Young African Sports Club. Hakiki ujio wa Mayanga umedhihirisha ubora wa Stars katika kunogesha utamu wa mechi hiyo.


KIKOSI CHA DAMU CHANGA.
Kwa mara ya kwanza Watanzania tunaitazama Stars ikicheza soka lenye ubora, lililo sheheni kila aina ya ufundi katika uwanja wao wa nyumbani. Hakuna wa kunibishia kuwa sababu kubwa ya hayo yote ni zile silaha za maangamizi zenye damu changa tulizo zimwaga pale uwanjani dhidi ya maadui zetu ‘The Zebras’.


Safu ya ulinzi ikiongozwa na kuimarishwa vyema na Abdi Banda, dimba likikamatiwa vizuri na Himid Mao Nkami pamoja na Frank Domayo ‘Chumvi’,  vilevile nahodha wa timu hiyo Mbwa Ally Samatta aliiongoza vyema safu ya ushambuliaji. Umahiri wa idara zote kwa Stars ulidhihirika kutokana na umri mdogo wa nyota wake.

UWEPO WA NAPE NNAUYE UWANJANI.
Katika vitu vitatu (3) vilivyo shangiliwa kwa nguvu ya furaha isiyo kifani na mashabiki wa soka waliofika uwanjani kushudia pambano hilo, cha kwanza ni goli la mapema la Stars lililo fungwa katika dakika y tatu na Samatta, cha pili ni ujio wa Mbunge wa Mtama, Mkoani Lindi, Mh. Nape Mosses Nnauye ambaye alikuwa Waziri mwenye dhamana ya michezo ambapo uteuzi wake ulitenguliwa alhamisi ya wiki hii na Rais Magufuli na nafasi yake kuchukuliwa na Dakta Harrison Mwakyembe, na cha tatu ni goli la pili na la mwisho kwa Stars ambalo lilifungwa na Samatta katika dakika ya 84.


‘SAPOTI YA MWAKYEMBE’
Kitendo cha uzalendo kilicho fanywa na Waziri mpya wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Dakta. Harrisn Mwakyembe kuhudhuria katika mechi hiyo kimeibua hamasa kwa wadau wa soka na mashabiki kwa ujumla na kupelekea timu ya Taifa kuibuka na ushindi mnono katika mchezo huo.

AMANI NA UPENDO.
Upendo na amani ni moja kati ya nguzo kubwa na kitambulisho cha Tanzania na Watanzania. Hakika mchezo ulikuwa wa kiungwana ndani na nje, hivyo amani na upendo vilitamalaki, na kufanikisha mambo kwenda sawa katika kila sekunde ya mchezo huo.

Ushindi wa mechi hiyo utaisaidia Stars kupanda katika viwango vya soka vya FIFA  kwa Afrika na duniani mara baada ya kumalizika kwa ratiba ya michuano hiyo ambapo kwa sasa Stars wakiwa katika nafasi ya 157 duniani,  wakati Botswana wakiwa juu katika nafasi ya 116 duniani.
Share on Google Plus

About BASEMENT255

0 comments:

Post a Comment