PROFESA LIPUMBA AIFUMUA CUF





MGOGORO mkubwa wa kisiasa unaoendelea kukitafuna Chama Cha Wananchi (CUF), umezidi kuchukua sura mpya baada ya Mwenyekiti wa chama hicho anayetambuliwa na Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, Profesa Ibrahim Haruna Lipumba, kutangaza kutengua uteuzi wa wakurugenzi sita.
Akizungumza Jumatatu ya Machi 06, mwaka huu na waandishi wa habari Makao Makuu ya chama hicho yaliyopo Buguruni jijini Dar es salaam, Profesa Lipumba aliwataja wakurugenzi hao kuwa ni pamoja na, Omari Ali Shehe (Mipango na Uchaguzi) na Salim Abdallah Bimani (Habari, Uenezi na Mawasiliano na Umma).

Wakurugenzi wengine waliyokumbwa na fagio hilo ni pamoja na Abdallah Bakari Hassan (Naibu Mkurugenzi wa Fedha na Uchumi), Pavu Juma Abdallah (Naibu Mkurugenzi wa Haki za Binadamu na Sheria), Yusuf Salim (Naibu Katibu Kamati ya Ulinzi na Usalama) na Mahmoud Ali Mahinda (Katibu Mtendaji wa Jumuiya ya Vijana)

Kwa mujibu wa Profesa Lipumba, uamuzi huo umetokana na viongozi hao kutotekeleza majukumu yao ipasavyo sambamba na kutohudhuria vikao mbalimbali kikiwemo kikao cha Kamati ya Utendaji kilichofanyika hivi karibuni licha ya kupelekewa taarifa mapema.

“Nimelazimika kufikia uamuzi huu kutokana na wakurugenzi hawa kutotekeleza majukumu yao ipasavyo na kutohudhuria vikao muhimu vya kikatiba”, amesema Profesa Lipumba.
Uamuzi huo wa Profesa Lipumba bila shaka utaendelea kukoleza moto wa mgogoro ndani ya chama hicho ambao kwa kiasi fulani unaonekana kuzalisha makundi makubwa mawili ya CUF-Bara na CUF-Zanzibar.

Taarifa zilizopatikana kutoka katika duru mbalimbali za chama hicho kikuu cha upinzani visiwani Zanzibar, zimeeleza kuwa wakurugenzi wote waliyotenguliwa nyadhifa zao, ni wafuasi sugu wa Katibu Mkuu wa chama hicho, Maalim Seif Shariff Hamad ambaye yupo katika mgogoro mkubwa na Mwenyekiti wake.


Hata hivyo Maalim Seif mwenyewe hakupatikana mara moja kuzungumzia maamuzi hayo ya kuwatimua kutoka katika nyadhifa zao wakurugenzi hao sita ambao misimamo yao imekuwa dhahiri ya kutomtambua Profesa Lipumba kama Mwenyekiti wa chama hicho.
Share on Google Plus

About BASEMENT255

0 comments:

Post a Comment